Friday, 13 April 2018

MO SALAH AVUNJA REKODI LIGI KUU UINGEREZA

Mo Salah ameshinda tuzo ya mchezaji bora wa mwezi Machi katika ligi kuu nchini England.

Amekuwa mchezaji wa kwanza kuwahi kushinda tuzo hiyo mara 3 ndani ya msimu mmoja.

DROO YA UEFA NUSU FAINALI

Je Madrid Kuendeleza Ubabe Mbele Ya Bayern?
Mohamed Salah Dhidi Ya Waajiri Wake Wa Zamani

DROO YA EUROPA NUSU FAINALI

Nani Kuaga? Nani Kwenda Fainali?

Thursday, 12 April 2018

SIMBA YAENDELEZA DOZI BILA ANGALIA MTU USONI

Kikosi cha Simba kimezidi kujikita kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara(VPL) baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya Mbeya City FC.

Mabao ya Simba yamefungwa na Emmanuel Anord Okwi, Asante Kwasi na John Bocco.

Mbeya City wamejipatia bao lao kupitia kwa Frank Ikobel na kuufanya mchezo umalizike kwa idadi hiyo ya mabao.

Simba wamefikisha alama 55 dhidi ya watani wao wa jadi Yanga walio na 47.

Mpaka sasa Simba imeshacheza jumla ya michezo 23 huku Yanga ikiwa na 22.

Vipi Kombe Litaenda Msimbazi Au Litaenda Jangwani?

KOCHA HANS VAN DER PLUIJM AMALIZANA NA AZAM FC


Kuna taarifa kwamba Kocha Mholanzi Hans van der Pluijm ameshamalizana na Azam FC ambayo ataanza kuinoa mara tu baada ya msimu huu kwisha.
Ligi imebakiza takribani mechi saba au nane kwa kila timu.

Inaelezwa kwamba kimyakimya Pluijm kamalizana na Azam FC.

"Kweli kocha amesaini mkataba wa miaka miwili na kila kitu safi, akimaliza msimu anaenda zake Azam FC," kilieleza chanzo.

Kwa sasa, Pluijm anainoa Singida lakini Yanga inaonekana ilipania kumpata Baada ya kuondoka kwa Kocha George Lwandamina ambaye amerejea kwao Zambia na kujiunga na Zesco tena.

Ingawa inaonekana kocha huyo asingependa kulizingumzia suala hilo mapema sana.

Kaa Karibu Zaidi Na Blog Yetu Kwa Taarifa Zaidi

Tuesday, 10 April 2018

Bodigadi wa Mayweather apigwa risasi Atlanta




Vyombo mbalimbali vya habari vimeripoti kuwa mtu mmoja anaedaiwa kuwa mmoja wa walinzi wa karibu wa bondia wa Marekani, Floyd Mayweather amepigwa risasi nje ya Hoteli ya Atlanta hapo jana asubuhi siku ya Jumatatu.

Mtandao wa habari za michezo wa TMZ Sports umeripoti kuwa kwamujibu wa taarifa za Polisi, risasi imetoka kwa mtu ambaye alikuwa kati ya moja ya magari matatu yaliyokuwa yamewasili nyuma ya hoteli ya InterContinental Buckhead majira ya saa 3 a.m. asubuhi siku ya Jumatatu.

Kwa mujibu wa chombo cha habari cha CNN kimeripoti kuwa mlinzi huyo ambaye jina lake halija fahamika amefikishwa kwenye Hospitali ya Grady Memorial kwaajili ya kupatiwa matibabu kufuatia risasi hiyo kumjeruhi mguuni na hali yake inaendelea vizuri.

Taarifa kutoka Polisi zinaeleza kuwa wanaamini bondia, Mayweather alikuwa sehemu ya msafara huo uliyoshambuliwa licha ya kutokuwa na uhakika kama yeye ndiye alikuwa mlengwa wa tukio hilo.

Hii ndio ratiba ya nusu fainali kombe la shirikisho

 

Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limewataarifu wapenzi wa soka nchini kuwa michuano ya kombe ya Shirikisho (ASFC) kwa hatua ya nusu fainali inatarajiwa kuanza kutimua vumbi mnamo Aprili 20 na 21, 2018 kwa timu nne zilizoweza kufuzu nafasi hiyo.

Hayo yamewekwa wazi na Afisa Habari wa TFF, Cliford Mario Ndimbo wakati alipokuwa anazungumza na waandishi wa habari Jijini Dar es Salaam na kusema nusu fainali ya kwanza itachezwa siku ya Ijumaa Aprili 20,2018 ikiwakutanisha Stand United ya Shinyanga watakaokuwa wenyeji wa Mtibwa Sugar ya Morogoro kwenye uwanja wa Kambarage Mkoani Shinyanga.

Aidha, Ndimbo amesema timu ya Singida United watawakaribisha JKT Tanzania kwenye nusu fainali ya pili itakayochezwa katika dimba la Namfua siku ya Jumamosi Aprili 21,2018.

Kwa upande mwingine, Ndimbo amesema washindi kwenye nusu fainali hizo watacheza mchezo wa fainali Mei 31, 2018.

Singida United yasema imejipanga vizuri kuikabili Yanga


Uongozi wa klabu ya Singida United, umesema utaingia uwanjani kwa tahadhari kubwa ukiamini Yanga watakuwa na hamu ya kulipa kisasi, kesho.

Singida United watakuwa wageni wa Yanga katika mechi ya Ligi Kuu Bara kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam, kesho.

Katika mechi ya mwisho, timu hizo zilikutana katika michuano ya Kombe la Shirikisho na Yanga kung’olea. Mechi ilipigwa mjini Singida.

Mkurugenzi wa Singida United, Festo Sanga amesema wako tayari na wamejiandaa hata kama Yanga watakuwa na hasira.

“Tumejiandaa na hatuna majeruhi, tunajua Yanga wataingia kama mbogo aliyejeruhiwa lakini sisi tuko tayari kwa mchezo na tunataka kufanya vizuri,” alisema.

Ronaldo ampa zawadi hii Rashford


MSHAMBULIAJI wa Manchester United, Marcus Rashford ameonyesha zawadi ya kiatu chekundu cha Nike Air Max 97 CR7 alichopewa na nyota wa Real Madrid, Cristiano Ronaldo.

Nyota wa zamani wa United, Ronaldo inawezekana hakuwa karibu na Rashford wakati wake anacheza Old Trafford kwani wakati huo Marcus alikuwa ana umri wa miaka 11 wakati Ronaldo alipokuwa anahamia Madrid – lakini wawili hao kwa sasa ni rafiki.

Kwa ushirikiano na Nike, Mwanasoka huyo bora wa dunia, Ronaldo ametoa kiatu hicho kikali kinachouzwa kwa Pauni 145, ambacho kinaweza kuwavutia mashabiki wengi wa Man United kununua.

Lwandamina aikimbia Yanga


KOCHA Mzambia, George Lwandamina ameondoka leo kwenda Zambia na habari zinasema anarejea Zesco United ya kwao na atatambulishwa Alhamisi.

Kaimu Katibu Mkuu wa Yanga, Charles Boniface Mkwasa amsema leo kwamba Lwandamina hajatokea mazoezini leo asubuhi bila sababu na wanamtafuta hapatikani.

“Mimi sijui kaenda wapi, kwa sababu hajaniaga. Hizo hizo habari (za kwenda Zambia) wewe ndiyo unaniambia,”amesema Mkwasa baada ya kuulizwa na Bin Zubeiry Sports – Online juu ya kocha huyo kurejea kwao, Zambia.

Habari zinasema kwamba Zesco United imeamua kumrejesha kocha wake huyo baada ya mafanikio yake Tanzania ndani ya miaka miwili, akiiwezesha kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara msimu uliopita na sasa inakaeribia kuingia hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika.

Yanga SC imejiweka kwenye nafasi nzuri ya kwenda hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho la Afrika baada ya ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Wolaita Ditcha ya Ethiopia katika mchezo wa kwanza wa mchujo wa kuwania kuingia hatua hiyo Jumamosi Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Ushindi huo uliotokana na mabao ya Raphael Daudi kipindi cha kwanza na Emmanuel Martin kipindi cha pili, unamaanisha Yanga SC watahitaji kwenda kulazimisha sare ugenini wiki ijayo, au kutofungwa zaidi ya tofauti ya bao moja ili kwenda hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho kwa mara ya pili baada ya mwaka 2016.

Na Lwandamina ambaye mkataba wake unamalizika Juni mwaka huu, anaondoka Yanga siku moja kabla ya kuteremka uwanjani kumenyana na Singida United katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Lwandamina alijiunga na Yanga Novemba mwaka 2016 akichukua nafasi ya Mholanzi, Hans van der Pluijm na katika kipindi hicho ameiongoza timu katika michezo 77 ya mashindano yote akitoa sare 18, kushinda 45 kati ya hizo mbili kwa penalti baada ya sare ndani ya muda wa kawaida na kufungwa 14, tano kwa penalti baada ya sare katika muda wa kawaida.

Manara aendelea kusisitiza Viwanja vya mikoani vina changamoto kubwa.



Afisa Habari wa klabu ya Simba, Haji Manara, ameendelea kusisitiza kuwa viwanja vingi vya mikoani vina changamoto kubwa.

Manara ameeleza kuwa viwanja hivyo vimekuwa na mapungufu mengi ambayo yamekuwa yakishindwa kuhimili vizuri mikiki-mikiki ya wachezaji na mpira pindi unapotandazwa Uwanjani.

Akizungumza mapema baada ya mchezo wa jana kati ya Mtibwa Sugar dhidi ya Simba, Manara alieleza kuwa asilimia kubwa ya viwanja mikoani si vizuri hivyo ni moja ya changamoto wanayopitia kama klabu na kwa wachezaji.

Mbali na Manara, baadhi ya wadau wa soka wamekuwa wakiongelea pia namna viwanja vingi vilivvyo nje ya Dar es Salaam kutoridhisha haswa katika sehemu ya kuchezea huku hakuna ukarabati mzuri ambao umekuwa ukifanyika ili viwanja hivyo viwe na hadhi nzuri kutumika.

TRA yakusanya Trilioni 11.78 katika kipindi cha miezi tisa



Mamlaka ya Mapato Tanzania imekusanya Tsh Tril 11.78 katika kipindi cha miezi tisa ya mwaka wa fedha 2017/18 kuanzia Julai 2017 hadi Machi 2018, ikilinganishwa na Tsh. Tril 10.86 ambazo zilikusanywa katika kipindi cha mwaka wa fedha 2016/17, ambacho ni sawa na ukuaji wa 8.46%.